MWENGE WA UHURU WAMULIKA MIRADI 7 KATIKA MANISPAA YA SHINYANGA
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mwenge wa Uhuru umemulika jumla ya miradi saba katika Manispaa ya Shinyanga, yenye thamani ya sh. bilioni 5.2.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, amebainisha hayo leo Agosti 19, 2026, wakati akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Peter Masindi.
Amesema, Mwenge ukiwa katika wilaya ya Shinyanga utatembelea jumla ya miradi 14, ambapo miradi saba iko katika Manispaa ya Shinyanga yenye thamani ya sh. bilioni 5.2, na miradi saba iko katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga yenye thamani ya sh. bilioni 5.4.
“Fedha zote hizo zimeletwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,” amesema Mtatiro.
Naye Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang’onda, akizungumza kwenye miradi hiyo, amesema Mwenge umefurahishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na umeridhia yote kuzinduliwa.
Aidha, Mwenge ukiwa katika Manispaa ya Shinyanga umekimbizwa umbali wa kilomita 84, ambapo umezindua mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji, kufungua Zahanati ya Kijiji cha Mwagala, kuweka jiwe la msingi katika Hoteli ya Makindo, kukagua shughuli za Kikundi cha Vijana cha Mkasa Fashion.
Miradi mingine ni kuzindua duka la nishati safi ya kupikia la kikundi cha wanawake cha Samia, kufungua daraja la Dodoma, kuzindua vyumba vinne vya madarasa na kuzindua Jukwaa la Vijana.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro kushoto akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Kishapu Peter Masindi.
Tags
HABARI












