SWEDEN, UNIDO KUCHOCHEA UKUAJI WA SEKTA YA MAZIWA SHINYANGA
Na Mapuli Kitina Misalaba
BALOZI wa Sweden nchini Tanzania, Ingrid Teresia Johansson, akiambatana na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Ms. Lorence Ansermet, wametembelea kiwanda cha Jambo Group mkoani Shinyanga kwa lengo la kujadili fursa za ushirikiano katika kuwawezesha wafugaji wadogo na kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa maziwa.
Ziara hiyo imefanyika leo Jumatatu, Novemba 16, 2026, ambapo viongozi hao wamejadiliana na uongozi wa kampuni hiyo kuhusu namna ya kuimarisha upatikanaji wa maziwa kutoka kwa wafugaji, kuboresha vituo vya kukusanyia maziwa pamoja na kuongeza uzalishaji viwandani.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amesema Serikali inathamini juhudi za kuimarisha mahusiano ya Tanzania na mataifa mengine, akieleza kuwa ushirikiano huo unaweza kufungua fursa zaidi za maendeleo ya viwanda na sekta ya ufugaji.
Mtatiro amesema kiwanda cha Jambo Group kina mchango katika kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, hususan maziwa, ambapo katika kipindi cha takribani mwaka mmoja na nusu uliopita kimepanua wigo wa uzalishaji kwa kuanza kuzalisha maziwa na bidhaa nyingine zinazotokana na maziwa.
Amesema kwa sasa kiwanda hicho kinaendelea na juhudi za kuhakikisha kinapata takribani asilimia 80 ya mahitaji yake ya maziwa kutoka kwa wafugaji wa ndani, huku akieleza kuwa ushirikiano na Sweden pamoja na UNIDO unaweza kusaidia kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Afisa wa Jambo Group Mussa Rioba, amesema ziara hiyo imelenga kujadili namna ya kuwawezesha wafugaji wadogo kuboresha ufugaji wao pamoja na kuimarisha vituo vya kukusanyia maziwa vinavyojulikana kama TENKAS ili viendane na mifumo ya kisasa.
Rioba amesema kiwanda kinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maziwa ya kutosha, hali inayosababisha uzalishaji kusimama kwa nyakati fulani kutokana na uhaba wa malighafi hiyo.
Amesema kwa sasa kiwanda kinazalisha takribani lita 30,000 za maziwa kwa siku, wakati mashine zake zina uwezo wa kuzalisha hadi lita 100,000 kwa siku, hivyo kuna umuhimu wa kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa maziwa ili kuhakikisha kiwanda kinakuwa na malighafi ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji endelevu.
Amesema maboresho ya vituo vya ukusanyaji wa maziwa yatasaidia kuongeza kiwango cha maziwa kinachokusanywa kutoka kwa wafugaji na kuhakikisha kiwanda kinaendelea na uzalishaji bila kusimama kutokana na upungufu wa malighafi.
Aidha Ms. Lorence Ansermet ni mwakilishi wa UNIDO anayesimamia shughuli za shirika hilo katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi, Mauritius, Seychelles na Umoja wa Visiwa vya Comoro.
Wawakilishi wa Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania, UNIDO, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga pamoja na viongozi wa Jambo Group wakielekea kiwandani kuanza ziara ya kutembelea na kujadili fursa za ushirikiano katika sekta ya ufugaji na uzalishaji wa maziwa.
Wawakilishi wa Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania, UNIDO, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga pamoja na viongozi wa Jambo Group wakielekea kiwandani kuanza ziara ya kutembelea na kujadili fursa za ushirikiano katika sekta ya ufugaji na uzalishaji wa maziwa.
Wawakilishi wa Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania, UNIDO, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga pamoja na viongozi wa Jambo Group wakielekea kiwandani kuanza ziara ya kutembelea na kujadili fursa za ushirikiano katika sekta ya ufugaji na uzalishaji wa maziwa.
Balozi wa Sweden nchini Tanzania, wawakilishi wa UNIDO na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga wakipokea maelezo kutoka kwa viongozi wa Jambo Group kuhusu shughuli za uzalishaji, uwezo wa kiwanda na mifumo ya ukusanyaji wa maziwa kutoka kwa wafugaji.
Viongozi wa Jambo Group, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, wawakilishi wa Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania pamoja na Shirika la UNIDO wakitembelea kiwanda cha Jambo Group mkoani Shinyanga kujadili fursa za ushirikiano katika kuimarisha sekta ya ufugaji na uzalishaji wa maziwa.
Balozi wa Sweden nchini Tanzania, wawakilishi wa UNIDO na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga wakipokea maelezo kutoka kwa viongozi wa Jambo Group kuhusu shughuli za uzalishaji, uwezo wa kiwanda na mifumo ya ukusanyaji wa maziwa kutoka kwa wafugaji.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akizungumza kuhusu umuhimu wa ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden katika kufungua fursa za maendeleo ya viwanda na kuwawezesha wafugaji.
Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Ingrid Teresia Johansson, akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea kiwanda cha Jambo Group mkoani Shinyanga, ambapo ameeleza fursa za ushirikiano katika kukuza sekta ya ufugaji na uzalishaji wa maziwa.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Ms. Lorence Ansermet, akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea kiwanda cha Jambo Group mkoani Shinyanga.
Afisa wa Jambo Group, Mussa Ribo, akielezea shughuli za uzalishaji kiwandani pamoja na changamoto ya upatikanaji wa maziwa ya kutosha kutoka kwa wafugaji.
Tags
HABARI










