HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA IMETOA FEDHA ZA MIKOPO SH. MILIONI 116.8 KWA VIKUNDI 10

HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA IMETOA FEDHA ZA MIKOPO SH. MILIONI 116.8 KWA VIKUNDI 10

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga imetoa mikopo ya Sh milioni 116.8 kutoka katika mapato yake ya ndani asilimia 10, kwa ajili ya kuviwezesha vikundi 10 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Hafla ya makabidhiano ya mikopo hiyo kwa njia ya mfano wa hundi, imefanyika leo Novemba 17, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, akizungumza kabla ya kukabidhi mfano wa hundi ya mikopo hiyo, amewataka wanakikundi kuzitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kukuza uchumi wao, badala ya kuzitumia katika mambo ya anasa.

Amesema, fedha hizo zimetolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mitaji ya kuanzisha, na kuendeleza biashara zitakazowakwamua kiuchumi, hivyo siyo fedha za kuzitumia vibaya.
Aidha, amewaonya viongozi mbalimbali, wakiwamo maofisa maendeleo ya jamii, kuacha tabia ya kuwaomba fedha wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, kwa kisingizio cha shukrani au hisani kwa kuwawezesha kupata mikopo hiyo.

Amesema, fedha hizo siyo za hisani, bali ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyeziagiza halmashauri kutenga na kutoa mikopo hiyo ili kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mitaji ya biashara na kuinua hali zao za kiuchumi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wanufaika hao kutokubali kutoa fedha zozote kwa viongozi au watendaji kama shukrani au hisani, badala yake wazitumie kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha wanazirejesha kwa wakati ili kuwawezesha wengine nao kunufaika.

Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Joseph Ntomela, amesema kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kuanzia Julai hadi Septemba, halmashauri hiyo imetoa mikopo ya Sh milioni 116.8 kwa vikundi 10, ambapo vikundi vitano ni vya wanawake, vitatu vya vijana na viwili vya watu wenye ulemavu.
Amefafanua kuwa vikundi vitano vya wanawake vimepata Sh milioni 57.3, vijana Sh milioni 45.5, huku vikundi vya watu wenye ulemavu vikipewa Sh milioni 14.

Kwa upande wao, baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo, akiwamo Yunis Silivester, wameishukuru Serikali na halmashauri kwa kuwapatia mikopo hiyo, huku wakiahidi kuitumia vizuri ili kujikwamua kiuchumi.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Andrew Mitumba akizungumza.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Joseph Ntomela akiwasilisha taarifa ya utoaji wa mikopo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akikabidhi fedha za mikopo kwa mfano wa hundi kwa wawakilishi wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Previous Post Next Post

نموذج الاتصال