KUMUOA BINTI WA KIHADZABE NI SHARTI USIFANYIWE TOHARA

Picha Mtandao
Kumuoa binti wa Kihadzabe ni sharti usifanyiwe tohara
KIONGOZI wa kimila wa kabila la Wahadzabe, Shaghembe Gambai amebainisha kwamba ili mwanamume aweze kufanikiwa kumuoa msichana anayetokana na jamii hiyo mojawapo ya masharti ni lazima uwe haujafanyiwa tohara.
Amesema kabila hilo linaamini kwamba kitendo cha mwanamume kufanyiwa tohara, hupunguza utaalam wa mambo na kufanya mwili wake kuwa legelege.
Kiongozi huyo wa jamii hiyo ya wawindaji, wavuna asali na waokota matunda wanaopatikana kwenye ukingo wa Ziwa Eyasi na Bonde la Ufa, amebainisha hayo leo akizungumza na Nipashe Digital katika Makumbusho ya Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai, maarufu kama UNESCO Global Geopark.
“Baadhi ya wanamume wanaotamani kuwaoa wasichana wa Kihadzabe hukwama, kwa sababu ya kushindwa kutimiza vigezo vinne, kikiwamo cha tohara, uwezo wa kula mizizi, matunda na nyamapori.
“Sisi Wahadzabe, tunaamini kuwa vitu hivyo hukupa nguvu ya kutosha na jembe la kazi wakati wa tendo la ndoa, huitaji kutafuta vumbi la Kongo (dawa ya asili inayodaiwa kuongeza nguvu za kiume) kama wala chipsi mjini,” anasema.
Ameongeza kuwa kigezo kingine wanachokiangalia ni uwezo wa kulenga shabaha, akisema Wahadzabe, wanaamini kwamba hutamlaza njaa binti yao, kila siku utarudi na nyamapori, ambayo ni chakula kikuu cha nyumbani.
Lakini pia kigezo kingine, mwanamume usiwe na mchepuko. Hiyo kwao ni ilani kwa mujibu wa Ghambai. Wanaamini mtu anayechepuka, anaweza kuuawa wakati wowote akifumaniwa kwa kuzini na pia kuleta maradhi nyumbani.
SOMA ZAIDI HAPA CHANZO NIPASHE.