RC MBONI MHITA AWATAKA WANAFUNZI KUONYESHA VIPAJI MICHEZO UMITASHUMTA
RC MBONI MHITA AWATAKA WANAFUNZI KUONYESHA VIPAJI MICHEZO UMITASHUMTA
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Wanafunzi wanaoshiriki michezo ya UMITASHUMTA kwa kuunda timu ya mkoa wa Shinyanga, itakayoshiriki mashindano ya kitaifa mkoani Iringa wametakiwa kuonyesha vipaji vyao.
Wito huo umetolewa leo Mei 23, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, wakati akifungua mashindano hayo yanayoshirikisha timu kutoka halmashauri sita za mkoa huo, kwa ajili ya kuunda timu moja ya mkoa itakayoshiriki mashindano ya kitaifa mkoani Iringa.
Mhita amesema, kwa sasa michezo ni ajira, hivyo amewasihi vijana hao kujituma kufanya vizuri kuonyesha vipaji vyao, kuwa na nidhamu ya hali ya juu pamoja na kuupatia ushindi mkoa huo.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa huo, CP Salum Hamduni, amesema michezo hiyo inashirikisha wanafunzi 710, na kwamba watachujwa kwa kuzingatia vipaji vyao ili kupata wanafunzi 120 watakaowakilisha mkoa katika mashindano ya kitaifa mkoani Iringa.
Mratibu wa michezo hiyo ambaye pia ni Afisa Utamaduni Mkoa wa Shinyanga Janeth Elias, amesema lengo la mashindano hayo ni kuibua na kukuza vipaji vya wanafunzi, na kwamba wamejipanga vizuri kurudi na ushindi.
Nao baadhi ya wanafunzi akiwamo Bugimbi Kashinje, wamesema wamejiandaa vizuri kushinda pamoja na kuonyesha vipaji vyao.
TAZAMA PICHA👇👇
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni akizungumza.
Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga Dedan Rutanzika akizungumza.