DIWANI WASHA AWASHUKURU WANANCHI WA MWAWAZA KWA KUMCHAGUA AHIDI MAENDELEO MAKUBWA
Na Mwandishi Wetu , SHINYANGA
Diwani wa Kata ya Mwawaza, Edwin Charles Washa, amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kata hiyo kwa lengo la kuwashukuru kwa imani waliyoonyesha kwa kumchagua kuwa mwakilishi wao, sambamba na kusikiliza kero zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga, Marium Nyangakalili, Diwani wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Mwanahamisi Kazoba, Mtendaji wa Kata ya Mwawaza, Naomi Stanley Kimaro, Afisa Elimu wa Kata hiyo, Elizabeth Mboje Samweli, Afisa Huduma kwa Wateja, Masaka Kabesha, Mhandisi wa TARURA, Eng. Kulwa Maige pamoja na Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Shinyanga Mjini, Saidi Bwaga.
Katika mkutano huo, wananchi walipata fursa ya kuwasilisha kero na maoni yao kuhusu huduma mbalimbali za maendeleo, huku viongozi waliokuwapo wakitoa majibu na ufafanuzi wa masuala yaliyoibuliwa ili kutafuta ufumbuzi.
Akizungumza na wananchi, Washa aliwashukuru kwa ushirikiano na imani waliyoendelea kumuonyesha, akiahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kushirikiana na wananchi pamoja na viongozi wa serikali katika kutatua changamoto zinazojitokeza.
Alisema ushirikiano kati ya viongozi na wananchi ni msingi muhimu wa kuharakisha maendeleo ya Kata ya Mwawaza na kuhakikisha huduma muhimu zinaboreshwa kwa manufaa ya wakazi wote.
Diwani wa Mwawaza Edwin Washa akisikiliza kero za wananchi.


















